Ala Za Muziki Katika Ibada

Na James M. Tolle (Mtafsiri Chris Mwakabanje)
Utangulizi:
1. Watu wengi wanapotembelea ibada za kanisa la Kristo kwa mara ya kwanza hustaajabia kitendo cha kutokuona ala za muziki ibadani.

2. Tunapaswa kuwa na majibu sahihi (1 Pet.3:15) kuhusu hili kama ilivyo katika mada mbalimbali zinazohusu Biblia.
a. Wasije wakadhani hatupendi tu kutumia vyombo vya muziki, au
b. Pengine, hatuna uwezo wa kununua ala za muziki.

3. Ala za muziki si miongoni mwa masuala yenye manufaa (expediency), bali ni mambo yanayogusa kanuni na taratibu (linga. 1 Kor.6:12).

4. Kanisa halifanyi mambo ambayo hulifurahisha, ama kufuata hekima za kibinadamu, bali kwa huzingatia mamlaka yatokayo juu (linga. Lk.20:1-8).

5. Je, Kristo ameamuru tutumie ala za muziki ibadani leo?
a. Tunapaswa kutambua ni wakati gani sheria inatufunga?
b. Je, maoni yana fungu gani katika ibada zetu?
c. Ni mambo gani yanachangia uimbaji bila kuvunja amri? (linga. 1Kor.6:12).

6. Kanisa la Kristo limefanya utafiti wa kina katika Neno la Mungu na kugundua kwamba hakuna amri, wala mfano wa Wakristo wakimwabudu Mungu huku wakitumia ala za muziki.
a. Kwa hiyo ni upotofu ambao haujatokana na mpango wa Mungu.
b. Kwa kuwa wanafunzi wengi wa Biblia wanashindwa kuthibitisha ndani ya Agano Jipya madai ya kutumia ala za muziki ibadani, basi aidha watakimbilia Agano la Kale au kwamba hakuna mahali Mungu amesema hapendi ala za muziki, n.k.

I. SHERIA YA IMANI

A. Tunaenenda kwa imani na wala si kwa kuona (2 Kor. 5:7).
1. Tunapata imani kwa njia ya kusikia neno la Kristo (Rum.10:17; Mt.17:5).

2. Kama tutafanya jambo bila kusikia kutoka ndani ya neno la Mungu, basi kibiblia hatuenendi kwa imani.

3. Pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu (Ebr.11:6).

B. Neno imba limetajwa mara 9, ukiondoa katika ufunuo lilivyotumika kwa namna ya mfano (Mt.26:30; Mdo.16:25; Rum.15:9; 1 Kor.14:14; Efe.5:19; Kol.3:16; Ebr.2:12; 13:15; Yako.5:13).

C. Hakuna shughuli yoyote inayolenga ibada itakayokubalika mbele za Mungu kama haijaagizwa naye.

1. Ibada inayokubalika mbele za Mungu inapaswa kuwa katika roho na kweli na wala si katika mwili, roho na kweli (Yoh. 4:24).
a. Ukweli ni neno la Mungu (Yoh.17:17).
b. Roho katika fungu hili ni utu wa ndani wa binadamu.

2. Tunapaswa kutofautisha huduma (service) na ibada (worship) – Rum.12:1-3.

3. Si kila kitu mwanadamu afanyacho ni ibada, kama Waislam wafundishavyo.

4. Ziko ibada aina nne:
a. Ibada katika roho na kweli (Yoh. 4:24)
b. Ibada ya kutungwa na wanadamu (Mt.15:8,9).
c. Ibada ya kujitungia (will-worship) – Kol.2:23. Matakwa ya mtu binafsi “arbitrary or self-devised worship.”
d. Ibada ya ujinga, huelewi mambo unayofanya ibadani (Mdo.17:22-28; Yoh.4:20-24).

D. Biblia inaagiza tunene mamoja wala pasiwepo na faraka kwa Wakristo (1Kor. 1:10).

1. Ikiwa Mungu anatuagiza kunia mamoja sisi kwa sisi na kuhitimu katika shauri moja; tukizingatia hayo ni vigumu tukatofautiana katika masuala ya msingi kabisa ya ibada (Filp.2:3-5; Rum.15:5).

2. Je, tunaweza kuwa na tumaini moja, imani moja, Bwana mmoja, Roho mmoja, ubatizo mmoja na Mungu mmoja, lakini si katika ibada moja? Efe.4:4-6.

3. Yesu aliliombea kanisa liwe na umoja, kama vile yeye alivyo na umoja na Baba (Yoh.17:20,21).

4. Watu hawajagawanyika katika masuala ambayo Yesu ameagiza, bali katika mambo ambayo hajaagiza. Hayo haswa ndiyo yanayotugawa kidini.
a. Hakuna anayepinga kuwa tunapaswa kuimba ibadani (Efe.5:19; Kol.3:16).
b. Mitume walifundisha mambo yote aliyoagiza Yesu (Mt.28:20; Yoh.16:13).
c. Roho Mtakatifu aliwaongoza mitume katika kweli yote. Ala za muziki si katika kweli yote aliyoifunua Roho Mtakatifu kwa mitume.
d. Mambo yote yafanyike kwa mamlaka ya Yesu Kristo (Kol.3:17).
i. Kuimba ni sharti kufanyike katika jina la Yesu, lakini kuimba pamoja na ala za muziki ni kinyume na mamlaka ya Yesu Kristo.
ii. Kwa kumjua (kujifunza) Kristo tumepewa mambo yote yapasayo uzima na utaua. Hatujifunzi popote Yesu na mitume wake wakitumia ala za muziki ibadani.

II. SHERIA YA IBADA
A. Kanuni za kweli za msingi kuhusu ibada ni muhimu sana kama ilivyo sheria ya imani; kwamba hakuna ibada yoyote itakayokubalika mbele za Mungu isiyoidhinishwa ndani ya Agano Jipya, Neno la Mungu.

B. Kanuni au sheria ya ibada imebainishwa katika Yoh. 4:24, “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

C. Ukweli ni nini? “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli” (Yoh. 17:17).

1. Kwa kuwa wanadamu wanapaswa kuabudu katika kweli, na neno la Mungu ndio kweli, hivyo basi, wanapaswa kuabudu kulingana na neno linavyosema.

2. Ni mahali gani ndani ya Agano Jipya panatuamuru tutumie vyombo vya muziki? Hakuna hata mahali pamoja!

3. Kuimba, ukijumuisha na ala za muziki ni kuvunja sheria ya ibada kinyume na tulivyoagizwa katika Yoh. 4:24.

III. HISTORIA

A. Ala za muziki ziliingizwa baadaye sana katika ibada kanisani (647 B.K.). Hata hivyo hazikutumika hadi kufikia karne ya nane.

1. Paul Henry Lang, “Music in Westen Civilization,” uk. 53, 54: “Vyanzo vyote vya habari vinataja uimbaji kanisani, lakini tahadhari ichukuliwe panapotajwa sanaa nyingine ya muziki… Maendeleo ya muziki Magharibi ni ushawishi uliotokana na uimbaji bila ala za muziki katika Kanisa la Kikristo.”

2. Kurt Pahlem, “Music of the World,” uk. 27: “Kuimba kwa kupokezana mistari – na neno “chant” (sio ala) limetumika, kwa karne nyingi zilizopita kabla ya ala za muziki kuingizwa katika tuni (melody).”

3. Hugo Leichtentritt, “Music, History and Ideas,” uk. 34: “Hata hivyo, kuimba tu, na si kupiga ala za muziki, kulikubalika katika kanisa la awali.”

4. Emil Nauman, “The History of Music, Juzuu 1, uk. 177: “Pasipo shaka kabisa uimbaji wa awali katika ibada takatifu kila mahali ulikuwa bila ala za muziki.”

5. Dr. Frederic Louis Ritter, “History of Music from the Christian Era to the Present, uk. 28: “Hatuna taarifa yoyote kabisa hasa ya namna ya uimbaji kanisani ulivyokuwa katika ibada za kidini katika makusanyiko ya Kikristo. Walakini, hata hivyo, tunaona kuwa ulikuwa uimbaji bila ala za muziki.”

6. Frank Landon Humphreys, “Evolution of Church Music, uk. 42: “Moja ya taswira inayotofautisha dini ya Kikristo na zingine nyingi ni utulivu wake; ilikusudia kudhibiti ishara zinazojitokeza nje kupitia hisia za ndani. Tabia zisizo za kiustaarabu, tena za dini ya Kiyunani, wakicheza na kuamasika kwa mitindo mbalimbali ili kudhihirisha hisia zao… Wakristo karne ya kwanza walijizuia kuonesha ishara za kusisimka, tangu mwanzo kabisa, muziki waliotumia, uliendana na msingi wa dini yao – utulivu wa utu wa ndani. Uimbaji uliotumika katika ibada zao awali kabisa ulikuwa ni kuimba bila ala za muziki.”

7. George Park Fisher, “History of the Christian Church, uk. 65, 121: “Awali kabisa uimbaji kanisani sehemu kubwa ulihusisha kuimba Zaburi, ukistawi haswa sehemu za Shamu (Syria) na Alexandria. Uimbaji ulikuwa wa kawaida kabisa. Palikuwa na aina nyingine za uimbaji katika ibada ya Wakristo, kama inavyoelezwa na Pliny. Katika Antiokia walianzisha uimbaji wakitumia ala (antiphony), mhusika ni Ignatius… Muziki wa kanisa la kwanza kabisa ulikuwa wa kwaya ukijumuisha kusanyiko zima.”

8. John Kurts, “Church History, Juzuu 1, uk. 376: “Awali kabisa uimbaji kanisani ulikuwa wa kawaida, usio wa kisanaa, wa kughani. Lakini kuibuka kwa uasi kulipelekea kanisa la Orthodox litilie manani sanaa zaidi. Chrysostom alipaza sauti dhidi ya kuigia kwa muziki wa kidunia kanisani. Upinzani uliendelea ukipinga ala za muziki kujumuisha katika uimbaji.”

9. Joseph Bingham, “Works,” London Edition, Vol, II, uk. 482-884: “Muziki kanisani ni wa zamani kama vile walivyo mitume, lakini ala za muziki si hivyo… Matumizi ya ala za muziki, hakika, ni suala la hivi karibuni, na si katika ibada za kanisa… Eneo la Magharibu, ala hazikutambulikana hadi karne ya nane; maana kinanda cha kwanza kuonekana Ufaransa kilipelekwa na Kostatino Kopronymus, mfalme wa Uyunani kama zawadi kwa Mfalme Pepin… Lakini, kilitumika ukumbini kwa binti wa mfalme tu, hakikuingizwa kanisani; wala ala za muziki hazikupokelewa kabisa katika makanisa ya Uyunani, hazitajwi mahali popote katika Liturugia, aidha la kale au hata la sasa.

10. Edward Dickinson, “Music in the History of the Western Church,” uk. 55: “Mtakatifu Ambrose anaonesha kuwadharau watu wanaopiga kinubi na zeze badala ya kuimba tenzi za rohoni na zaburi; na Mtakatifu Augustine anawataka waumini wasikengeuke mioyoni mwao kwa kufuata ala za muziki. Miongozo ya kidini kwa Wakristo wa awali haikukubaliana na hilo (incongruity), na hata kuona ni kufuru, kutumia vitu ambavyo huamsha ashiki, matokeo ya ala za muziki kwa mambo yasiyoonekana, ibada ya kiroho. Shauku yao kuu kidini na kimaadili si kuongeza vichocheo vya nje; uimbaji bila ala ulikuwa ndio njia pekee ya kuelezea imani yao.”

B. Psallo na Psalmos

1. Kuna watu wanaojaribu kutetea matumizi ya ala za muziki ibadani kwa kutaja neno “psallo,” kwamba maana ya neno hili linauhusiano na ala za muziki.

2. Neno “psallo” limetokea mara tano katika Agano Jipya (Rum.15:9; 1 Kor.14:15 (mara mbili hapo); Efe.5:19; Yak.5:13, bila kuwa na maana tofauti kabisa, tafsiri (versions) zote zinazokubalika – King James, English Revised, American Standard, na Douay (Roman Catholic) – hulitafsiri neno “psallo” kuwa “imba, imba zaburi, imba sifa, lahani au tuni (melody).”

a. Hakuna hata tafsiri moja inayotafsiri kuwa ni kupiga ala za muziki.

b. Hata tafsiri maarufu za kisasa za siku hizi (Goodspeed, Weymouth, Moffat, na Knox) zote zinatafsiri “psallo” kimsingi sawa na hizo tafsiri zinazokubalika.

c. Watu waliotoa tafsiri hizo zote ni miongoni mwa watu waliobobea kitaaluma katika lugha ya Kiyunani, wangetafsiri kuwa ni ala kama ingemaanisha hivyo.

3. Moulton na Milligan, walioandika moja ya kamusi zinazotegemewa na kuaminiwa, wakishughulikia Kiyunani cha Agano Jipya, hulitafsiri neno “psallo” kama lilivyotumika katika Agano Jipya: kuimba tenzi za rohoni.”

4. Abbott-Smith anachangia akithibitisha maana iyo hiyo: “…katika A.J. kuimba tenzi za rohoni, kuimba sifa.” Uthabiti wa maelezo ni wa kweli tunapoangalia mazingira yaliyotumika ya “psallo” na waandishi wa A. J; maana mjadala si juu ya matumizi ya neno, bali lilimaanisha nini kwa waandishi walioandika Agano Jipya.

5. Matumizi ya neno katika Yakobo 5:13 ni mfano dhahiri kuonesha kwamba waandishi wa Agano Jipya hawakuwaza kabisa akilini mwao suala la ala za muziki kwa neno hilo: “ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi [psallo].” Kuimba, muziki bila ala za muziki, ni namna ya kudhihirisha furaha na shamrashamra, jambo ambalo wanadamu wanao uwezo wa kufanya hivyo katika maisha ya kila siku.

a. Kama neno “psallo” lilivyotumika katika Yakobo lingemaanisha ala za muziki, basi ili mtu mwenye moyo wa kuchangamka atii ingemlazimu kutafuta ala za muziki bila kujali yuko wapi – kazini, michezoni, nyumbani au akiwa safarini.

b. Maneno (Efe.5:19) “kumshangilia Bwana mioyoni mwenu” – Kiyunani “psallontes” kutoka neno “psallo.”

c. Katika Kol.3:16, “huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu ni sawa na “kumshangilia Bwana mioyoni mwenu.”

d. Nomino inaoungana na “psallo” ni “psalmos” iliyotafsiriwa kuwa zaburi katika Agano Jipya.

e. Dr. Marvin R. Vincent, akiandika katika “World Studies of the New Testament, uk. 506, anatoa maoni yafuatayo kuhusu matumizi ya neno zaburi katika Agano Jipya: “Zaburi asilia ziliimbwa zikiambatana na ala za muziki za nyuzi. Dhana ya kujumuisha ala za muziki ikapitwan na wakati, kisha kutajwa kwa neno zaburi katika Agano Jipya ni zaburi za Agano la Kale au utenzi wenye sifa hizo.”

f. Bagster anasema hivi kuhusu “psalmos,” “nyimbo takatifu, zaburi, 1 Kor.14:26; Efe.5:19;” n.k.

g. Mfano mwingine wa matumizi ya neno “psalmos” ni katika Luka 20:42, “Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi…” Kama waandishi wangemaanisha “psalmos” kuwa ala za muziki, basi ingetafsiriwa hivi: “Maana, Daudi mwenyewe katika chuo cha kupiga ala za muziki, au chuo cha zaburi kutafsiriwa kwa kujumuishwa na ala za muziki. Kufikiri hivyo ni upuuzi!”

i) Kanisa la awali lilikuwa likifahamu vema Kiyunani na lilitumia lugha ya Kiyunani (hata Agano Jipya liliandikwa katika lugha hiyo), hawakuona vema neno “plasmos” na “psallo” kutafsiriwa kuwa ala za muziki.

ii) Wasomi walioandika kamusi za Kiyunani hawajatafsiri maneno “psalmos” na “psallo” kuwa ni kupinga ala za muziki.

iii) Waliotoa tafsiri (versions) maarufu pamoja na hizo zinazopendwa sana za kisasa, hawajatafsiri maneno “psalmos” na “psallo” kuwa ni ala za muziki.

iv) Kama maneno hayo yangemaanisha kupiga ala za muziki, basi kila Mkristo angepaswa kupiga ala za muziki kulingana na Efe.5;19 “Mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu.” Na katika Kol.3;16, “Mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni…”

IV. SABABU WATOAZO KUTUMIA ALA ZA MUZIKI

A. Hudai Agano jipya halisema ni makosa kutumia ala za muziki.
1. Katika chakula cha Bwana tumeamuriwa mkate usiotiwa chachu na mzao wa mzabibu. Je, ni sahihi kutumia nyama na viazi kwa sababu Bwana hajasema msitumie nyama na viazi mahali popote katika Agano Jipya?

2. Mungu alipowaambia Walawi wachukue moto madhahabuni kwa ajili ya kufukizia uvumba hekaluni, kwa kutaja hivyo alizuia moto mwingine wowote kutoka mahali popote pale (Law.10:1-2; 16:11,12).

3. Mungu ameagiza katika Agano Jipya tuimbe, mambo aliyonyamaza si ruhusa kwetu kabisa kuyafanya.

4. Kufundisha mambo ya Agano ya Kale ni kinyume na jinsi mitume walivyoamuriwa kufundisha, “Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi [mitume] hatukuwaagiza” (Mdo.15:24). Lazima tuheshimu Maandiko yanaponyamaza.

B. Watu hudai kwamba kwa kuwa Agano la Kale walitumia ala za muziki kwa nini leo tusitumie?
1. Yesu aliigongomelea torati msalabani na kuifuta isiwepo tena (Kol.2:14).
2. Leo, kanisa halimsikilizi Musa, bali Kristo (Yoh.1:17; Mt.17:5; 28:18).
3. Agano Jipya ni bora kuliko Agano la Kale (Ebr.8:6).
4. Ikiwa mtu anapenda kutumia vyombo vya muziki, basi inampasa kushika torati yote (Gal.3:10; Kumb.27:26; Law.18:5, n.k.).

C. Madai mengine ni suala la kuchangia tu uimbaji!
1. Wanaotoa madai haya hushindwa kutofautisha maneno kuchangia na kuongeza katika maagizo ya Mungu.

2. Neno mbao ni la jumla/ainasafu (generic). Kuna majina ya kipekee mengi kutoka ainasafu hiyo yanayobainisha mbao, kwa mfano mninga, mvule, msonobari, n.k.

3. Mwanzo 6:14, Nuhu aliambiwa atumie mvinje; kwa kuwa miti ni mingi duniani, unadhani angempendeza Mungu angetumia mti wa mninga, msonobari, mvule, n.k.?

4. Nuhu alifanya kila jambo aliloamuriwa na Mungu kikamilifu (linga. Mwa.6:22). Angetumia mti mwingine asingekuwa amechangia katika amri ya Mungu, bali angeongeza.

5. Mungu ametuagiza kuimba, unadhani atapendezwa tukiongeza kucheza, kupiga makofi, kupiga ngoma, gitaa, zeze, vinubi, n.k.?

6. Mungu hapendi wakati wote wanadamu waongeze wala kupunguza katika sheria zake (Kumb.4:2; 12:32; Mith.30:5,6; Ufu.22:18,19; 1 Kor.4:6).

7. Neno muziki ni neno la jumla/ainasafu. Kama Mungu angesema katika Agano Jipya pigeni muzika katika ibada, tungekuwa na uchaguzi: (1) muziki wa ala (2) sauti za vinywa vyetu, au (3) ala za muziki zikiambatana na sauti za binadamu.

8. Vitu vifaavyo, visivyo haribu amri ya kuimba ni: vitabu vya nyimbo, uma wa tuni (pitch pipe), kupanga sauti, pamoja na vyote visivyovunja amri ya kuimba.

9. Ala za muziki huwakilisha tendo lingine katika uimbaji tofauti kabisa na kutumia vitabu vya nyimbo, maiki, spika, n.k.

10. Mnyama ni neno la jumla/ainasafu (generic). Kuna wanyama wengi katika ainasafu hiyo kama vile: farasi, ng’ombe, kondoo, n.k.

a) Katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, Mungu aliwaagiza mnyama wa kutoa – mwana kondoo (Kut. 12:5).

b) Je, wasingevunja sheria kama wangetumia mnyama mwingine?

c) Au, ingekuwaje kama wangechinja mwanakondoo wakati wa Pasaka pamoja na wanyama wengine wasioagizwa?

11. “Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze” (Kumb. 12:32).

D. Wengine hudai kuna ala za muziki mbinguni, kama alivyoona Yohana (Ufu.5:8; 14:1,2; 15:2).
1. Iwapo tutachukulia “wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne … kila mmoja wao ana kinubi…” (5:8), kuwa ni lugha nyepesi ya kawaida, basi tunapaswa kutafsiri kuwa vitu halisi: wenye uhai wanne, wazee ishirini na wanne, sauti ya radi, vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, mwanakondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto!” (neno ‘kama’ huashiria tashibiha) – “kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu, … kama sauti ya wapiga vinanda (14:2).

2. Suala hilo lingekuwa ni sahihi, basi tungengojea kufika mbinguni na kushuhudia ala hizo Mungu alizoziweka huko. Hapa mada yetu ni jinsi gani tumeagizwa kuimba kanisani! Kuna uhusiano gani mambo ya mbinguni na yale tuliyoagizwa hivi sasa kanisani?

E. Wengine hudai ala za muziki tunazofurahia majumbani kwa nini tusifurahie kanisani?
1. Kuna mambo mengi ambayo ni halali kufanyika majumbani, lakini hayawezi kufanywa ibadani; k.m. kuosha mikono, kula chakula, kuangalia Runinga, burudani mbalimbali, n.k.

2. Je, tuingize masuala ya majumbani mwetu katika ibada kwa Mungu? (linga. Kumb.12:13, 15).

F. Wengine hudai, makusanyiko yana watu wenye vipaji vya kupiga ala za Muziki, kwa nini tusiwatumie?
1. Vipi kuhusu wapishi wazuri wa keki watuandalie keki kwa ajili ya chakula cha Bwana?

2. Unaonaje kuhusu vijana wenye vipaji vya kuchekesha tuwatumie ibadani, watuburudishe badala ya kusikiliza mafundisho ya Biblia?

Ubatizo Wa Watoto

Je! Tuwabatize Watoto Wachanga?

Na: Larry Ritter

 

Watu wengine katika dini zao wana kawaida ya kubatiza watoto wadogo. Lakini Biblia inasemaje kuhusu hilo? Je! Hivyo ndivyo Mungu apendavyo? Je! Yesu alifundisha lolote kuhusu lilo? Je! Upo mfano wowote katika Biblia ambapo mtoto alibatizwa?

Kama kawaida tunapaswa kupata maelekezo na mifano kutoka kwenye maneno ya Mungu Biblia (2 Tim. 3:16-17), “Kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho na kwa kuaonya watu makosa yao na kuwaongoza na kuwaadabisha katika haki ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda haki.”Biblia ndio nguvu yetu na mamlaka ya mwisho katika mambo yote ya kiroho. Tuangalie na tuone Mungu anasemaje kuhusu ubatizo.

1.Warumi 10:17, Paulo anasema, “Imani huja kwa kusikia na kusikia huja kwa neno la Mungu.” Je! Mtoto mchanga anaweza kusikia neno la Mungu kwa kufundishwa na akakubali kwa kumwamini Mungu?

2. Marko 16:15, 16, Yesu anasema, “Nendeni ulimwenguni kote mkahubiri injili kwa kila kiumbe, atakayeamini na kubatizwa ataokolewa, asiyeamini atahukumiwa.” Je! Mtoto mchanga aweza kuamini? Je! Wanao uwezo wa kusikia injili, kufikili hilo na wakaamini?

3. Matendo 2:38, Hapa Petro alikuwa akiwaambila watu waliosikia na wakachomwa mioyo yao na walipouliza tufanye nini Petro aliwaambia, “Tubuni mkabatizwe katika jina la Yesu Kristo kwa ondoleo la dhambi.” Je! Vitoto vichanga vinaweza kutubu, au kubadili njia zao? Kama ndivyo wata tubu nini? Ama ubatizo ni nini? Petro anasema hapa kwa ondoleo la dhambi. Je! Watoto wanayo dhambi inayohitaji kuondolewa? Hapana, watoto wadogo hawana dhambi, watoto wanafahamu jema na baya? Hapana.

4. Matendo 8:12, “Na walipoamini Filipo akahubiri mambo ya husuyo ufalme wa Mungu na jina la Yesu Kristo, wakabatizwa nao wana wake na wanaume.” Tena hapa watoto waweza kuamini walichohubiliwa?

5. Matendo 8:36-37, Hapa Filipo alikuwa akimhubiria mtu mmoja kuhusu Yesu wakafika penye maji naye akasema, “Maji si haya, ni nini kitakochonizuia nisibatizwe? Naye Filipo akasema, ukiamini kwa moyo wote inawezekana, naye akajibu akasema, Naamini kuwa Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu.” Kabla ya mtu kubatizwa anapaswa kuamini kwa moyo wake wote. Je! Mtoto mchanga aweza kufanya hivyo?

6. Matendo 16:30-34, Mlinzi wa geleza alipotaka kujua afanya nini ili aokolewe Paulo na Silasi walimwambia, “Mwamini Bwana Yesu Kristo nawe utaokoka na nyumba yako.” Hapa walikuwa na maana ya kwamba nyumba yote ingeokoka kwa imani ya yule mlinzi? Angalia neno linaongelewa kwa wote waliokuwamo kwenye nyumba, inasema “yeye na wote wakabatizwawakati huo huo. Je! Inasema yeye alikuwa na watoto wachanga? Kwa hiyo tuamini alikuwa na watoto wachanga wakati Biblia haisemi?

7. Mathayo 18:1-5, Watu wengine wanachukua kipengele hiki kama mamlaka ya kuwabatiza watoto. Kwanza kabisa ubatizo haujatajwa popote hapa katika kifungu hiki cha maandiko. Wala haikuwahi kufikiliwa. Pia isingewezekana wabatizwe katika mauti (Rum. 6:3-5) hata hivyo katika swala hilo hata Yesu mwenyewe alikuwa bado hajafa.

Lakini kwa nini Yesu alifanya hivyo ni kwamba wanafunzi wake waaje kujilinganisha kuwa ni yupi mkubwa kati yao, walihitaji kunyenyekea kama mtoto mdogo. Utu wa mtoto ndio unaongelewa hapa. Huyo mtoto hakubatizwa.

Kwa kuhitimisha ni kwamba ubatizo sio kwa watoto. Ubatizo sio kwao ambao hawajakuwa bado kufahamu mema na mabaya. Ubatizo ni kwa wale tu walitenda dhambi na wanahitaji ondoleo la dhambi. Wachanga hawana dhambi, hawajitambui wenyewe, hawawezi kuamini. Kama hawaamini, kwa nini wabatizwe? Kama watoto hawaamini kabla ya kubatizwa kwa nini mtu mwingine afanye badala yao? Kwa nini wanafaunzi wa kwanza walifundisha nyumba kwa nyumba (Mdo. 20:20) kama kuamini sio muhimu? Je! Itakuwaje endapo mtu mzima akikataa kubatizwa? Utambatiza tu hata japo yeye hataki? Inakuaje sasa kwa watoto ambao hata hawajui kinachoendelea. Watoto hawahitaji kubatizwa.

                                        

KANISA LA KRISTO

‘KUAMINI’ MAANA YAKE NINI?

Tags

,

‘KUAMINI’ MAANA YAKE NINI?

“Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe nauzima wa milele” Yohana 3:16. Mstari huu ni moja ya mistari inayopendwa katika Biblia, na bado ni moja ya mistari ya Biblia iliyokosewa kueleweka. Sintofahamu hiyo hutokana na watu kuchanganya maana ya “kuamini”. Wengine hufundisha kuwa neno “amini” hapa humaanisha tu kumtambua Yesu kama mwokozi, na kwamba endapo wakifanya hivyo wanakuwa kwenye hali ya kuokolewa.

Neno “amini” katika Yohana 3:16 hutokana na neno la Kiyunani pisteuo, linalomaanisha ushawishi, tumaini la furaha, muunganiko wa utiifu. Neno “amini” katika Agano Jipya mara nyingi hubeba dhana ya utii. Neno hili pekee yake halimaanishi “saini ya kifikra.”

Mtu anaweza kutazama mazingira ambayo waziwazi Yohana 3:16 huangukia na ataweza kuona ushahidi kwamba katika mstari huu Yesu alimaanisha mambo mengi zaidi ya saini ya kifikra. Mazingira yenyewe ni Yohana 3:1-21. Na katika mistari hii twajifunza mambo matatu ambayo nataka kuyazingatia:

  1. Ili mtu awe ndani ya Yesu, ni lazima azaliwe mara ya pili, kuzaliwa kwa maji na kwa roho, Yohana 3:1-8.
  2. Katika Yohana 3:14 kuna nukuu ya Musa kumwinua nyoka jangwani. Hata kale, waliomtenda Mungu dhambi, hawakukaa tu nyumbani huku wakiamini kuwa yule nyoka wa shaba angewaokoa. Kimsingi walitakiwa kuinuka, kutembea kutoka hemani mwao, ambapo yawezekana ilikuwa ni umbali wa maili kadhaa (kumbuka kulikuwa na kambi ya watu wapatao milioni tatu) ili kufika mahali palipokuwa na yoka wa shaba ili kumtazama ili wawe hai, Hesabu 21:9. Ni wazi kwamba katika wokovu wao kulikuwa na zaidi ya saini ya kifikra

3) Yesu alidhihirisha kwamba endapo unataka kuijia nuru, kulikuwa na jambo ambalo mtu ulitakiwa kulifanya, “Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru,” Yohana 3:21.

Tuelewe kutokana na Neno la Mungu kuwa imani ya Kibiblia huhusisha imani inayompelekea mtu kutumaini na kutii. Kushindwa kutumaini na kumtii Yesu ni kushindwa dhahiri kumpokea kama Bwana na mwokozi. “Na kwanini mwaniita Bwana, Bwana, walakini hamyatendi nisemayo?” Luka 6:46

Kunyunyizia, Kumwagia, Au Kuzamisha – Ni Upi?

Tags

, ,

I. UBATIZO WA MAJI UMEAMRIWA.

a. Mt. 28:19, “Basi, enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu mkiwabatiza kwa jina la Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.”

b. Mdo. 2:38, “Petro akawaambia, tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu….”

c. Mdo 10:48, “Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo.”

d. Mdo. 18:8, “..na Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.”

e. Mdo. 22:16, “Basi, sasa unakawilia nini? Simama ubatizwe ukaoshwe dhambi zako..”

f. Rum. 6:3, “Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika kristo yesu tulibatizwa katika mauti yake.”

g. Hapa tumekwisha kuona jinsi Kristo na mitume walivyoamuru ubatizo kama ni kanuni ya wokovu (au ondoleo la dhambi) na kwa kuongozwa na Kristo.

II. NI AKINA NANI WANAOHUSIKA KUBATIZWA?

a. Ni wale wanaoweza kufundishwa, Mt. 28:18-20.

b. Ni wale wanaoamini, Mk. 16:15-16.

c. Ni wale waliotubu, Mdo. 2:38.

d. Ni wale waliomkiri, Mdo. 8:37. “Filipo akasema, ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana akajibu, akanena, naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.”

e. Watoto wadogo sio somo la ubatizo.  Hawajapotea; mtu hawezi kuokolewa kama hajapotea. Watoto wadogo hawajapotea wako salama hawana dhambi, Eze.18:20.  Pia, Watoto wadogo hawawezi kuamini, kutubu, au kumkiri Kristo, Mdo. 2:37.

III. WENGINE WALIBATIZWA TENA KATIKA AGANO JIPYA?

a. Paulo aliwakuta watu waliobatizwa ubatizo wa Yohana kabla ya sheria za Kristo kukamilika, Mdo. 19:3.

b. Kwa mafundisho ya Paulo, waliona inawalazimu kubatizwa tena kwa jina la Bwana Yesu; na kwa madhumuni aliyoyaeleza Kristo.

c. Wengi siku hizi wamebatizwa kwa njia isiyo sawa au kwa madhumuni yasiyo sawa; hawa wanapaswa kubatizwa kwa ondoleo la dhambi, Mdo. 2:38; Rum. 6:1-11.

IV. KUNYUNYIZIA, KUMWAGIA AU KUZAMISHA NI UPI?

a. Ubatizo ni kuzika: “Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu,” Kol. 2:12.

b. Ubatizo unahitajika. 1) Maji mengi, Yoh. 3:23. 2) Ni kutelemka majini, Mdo. 8:38. 3) Ni kuzama ndani ya maji, Mdo. 8:38. 4) Ni kupanda toka majini, Mt. 3:16. Yesu alibatizwa (kuzamishwa) na Yohana, si kwa ondoleo la dhambi, lakini ni kwa kuitimiza haki yote. Kwani Yeye hakuwa na dhambi.

c. Katika neno la Mungu “Ubatizo.”  1) “Ubatizo” tafsiri ya Kiyunani katika Agano Jipya ni baptizo. Neno hili linaeleza maana yake ni kutumbukiza, ni kuzamisha, na kadhalika.” 2) “Kunyunyiza” tafsiri ya Kiyunani katika Agano Jipya ni “Rantizo;” na kumwagia ni “Cheo”. 3) Mahali popote ambapo neno “ubatizo” linaonekana au kusemwa au kuandikwa ni baptizo sio rantizo au cheo.

V. Historia ya Affusio kunyunyizia au kumwagia (Kanisa lilianza mwaka 33 B.K.).

a. Mageuzi haya yaliandikwa mnamo 251 B.K. alipokuwa amelala kitandani kwa ajili ya ugonjwa.

b. Hapo kwanza, Affusio ilikuwa ikubaliwe na watawala kwa udhaifu.

c. Baraza la Ravenna, wakati wa 1311 B.K. liliutambua ubatizo wa kunyunyiza katika kanisa Katoliki.

d. Affusio ni uzushi wa wanadamu, ambao hauwezi kutimiza mpango wa Mungu wa wokovu.

VI. Kusudi la Ubatizo wa Agano Jipya.

a. “Unawaokoa ninyi pia siku hizi,” 1 Pet. 3:20-21.

b. Na matokeo yake ni msamaha wa dhambi, Mdo. 2:38.

c. “Unasafisha dhambi,” Mdo. 22:16.

d. “Unatuweka ndani ya Kristo,” Gal. 3:36-27.

e. Tulibatizwa “katika mauti ya Kristo,” Rum. 6:3-4. Kristo alimwaga damu kwa mauti yake, Yoh. 19:32-37. Tulibatizwa katika mauti yake. Ni katika ubatizo unaposhiriki damu ambayo husafisha dhambi zetu.

http://www.kanisalakristo.com

Biblia Yasema Nini…..Kuhusu Petro?

Tags

, ,

Yesu alipomchagua Simoni alimpa jina jingine la lugha ya Kiaramu akamwita Kefa. Maana yake katika Kiswahili ni jiwe (Yn. 1:40-42). Walakini lugha ambayo ilikuwa ikutumika zaidi katika siku za mitume ilikuwa Kiyunani. Katika Kiyunani jina Kefa linafasiriwa kuwa Petro. Watu wa siku zetu wamezoea sana jina Petro na, kwa hiyo, wengi wetu tumesahau kwamba katika Biblia Kefa na Simoni Petro ni mtu mmoja tu.

Petro na Mke Wake

“Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia (Yesu) habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.” Mk. 1:30-31.

Mistari hii inaonyesha kwamba Petro alikuwa ameoa mke. Watu fulani hudhani kwamba mke wa Petro alikuwa amekufa kabla Yesu hajamchagua. Wazo hili si kweli. Mke wa Petro alikuwa akifuatana naye katika kazi yake. Maana Paulo aliuliza, “Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa (Yaani Petro)?” 1 Kor. 9:5.

Petro na Funguo za Ufalme

Tangu mwanzo, Petro alikuwa hodari sana katika kunena. Hata Yesu alipokuwa akiongea na mitume, mara kwa mara alikuwa ni Petro ambaye alitangulia kumjibu. Huenda ujasiri huu wa Petro ndiyo maana Yesu alimwambia katika Mathayo 16:19 kwamba atapewa “funguo za ufalme .” Basi, siku ya Pentekoste, Petro alitumia funguo hizo akiwaambia watu: “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu…… Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa… Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa”. Mdo. 2:38, 41, 47.

Watu waliookolewa waliingizwa katika Kanisa ambalo ndilo ufalme (soma Kol. 1:13-14 na Yn. 3:5). Basi, baada ya Petro kuufungua ufalme (Yaani, Kanisa) siku ya Pentekoste, Petro hakumwachia mwanadamu mwingine funguo hizo. La! Bali funguo zilirudi kwa Yesu huko Mbinguni. Soma maneno ya Yesu kwa Kanisa la Filadelfia katika Ufunuo 3:7-8.

Petro na Msingi wa Kanisa

Katika Mt. 16:18 Yesu alisema: “Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”

Kwa sababu ya maneno hayo, baadhi ya watu husema kwamba Petro ni mkuu na msingi wa Kanisa. Walakini Yesu hakusema kwamba Kanisa litajengwa juu ya Petro tu. La! Maana katika Efe. 2:20-22 twasoma “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika Yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika Yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika roho.”

Paulo alisema: “Maana sisi (mitume) tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi (Paulo) kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mweingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani Yesu Kristo,” 1 Kor. 3:9-11.

Mistari hii ya Biblia inaonyesha wazi wazi kwamba Kanisa limejengwa juu ya msingi wa mitume wote, wala si Petro tu. Tena msingi ule wa mitume haukuwa ni Petro bali ulikuwa Yesu mwenyewe. Kumbuka, katika Mathayo 16:18 Yesu hakusema kwamba atalijenga Kanisa juu ya jiwe (Petro) bali juu ya mwamba. Mwamba huu ni ukweli ule alioutaja Petro katika Mt. 16:16 alipomwambia Yesu, “Wewe ndiwe Kristo, mwana wa Mungu aliye hai.” Kwa hakika Kanisa limejengwa juu ya mwamba (ukweli) huu, maana mtu hawezi kuingia katika Kanisa bila kuamini kwanza kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

Petro na Mitume Wengine

Katika Mt. 16:19 Yesu alimwambia Petro “….Lo lote utakalo lifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Baadhi ya watu hudhani kwamba maneno hayo yalimfanya Petro kuwa mkuu kuliko mitume wengine. Walakini, wazo hili si kweli. Maana katika Mt. 18:18 Yesu aliwaambia mitume wote: “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”

Yesu hakutaka kumfanya mtume mmoja awe mkuu kuliko wengine. Ebu! Tuone, siku moja mitume Yakobo na Yohana waliomba cheo kwa Yesu. Twasoma: “Wakamwambia, utujalie sisi tuketi mmoja mkono wako wa kuume na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako… Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. Yesu akawaita, akawaambia, mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa nguvu na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.” Mk. 10:37, 41-44.

Tena, twasoma: “Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, amin, nawaambia msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi ye yote ajinyen- yekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt. 18:1-4.

Petro na Uchungaji wa Kanisa

Watu wengine husema kwamba Yesu alimfanya Petro kuwa mkuu wa Kanisa alipomwambia “chunga kondoo zangu,” (Yn. 21:16). Walakini kazi hii ya kuchunga haikutolewa kwa Petro tu. La! Bali ni kazi ya wazee wote wa Kanisa (Mdo. 20:17, 18, 28). Petro mwenyewe amethibitisha ukweli huu, maana aliandika barua kwa wakristo akisema:

“Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni Kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa kwa moyo….. Na Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.” 1 Pet. 5:1, 2, 4.

Katika mistari hii Petro alionyesha wazi wazi kwamba hapakuwa na tofauti kati yake na wazee wengine wa Kanisa. Tena, alionyesha kwamba Mchungaji Mkuu ni Yesu atakayedhihirishwa kutoka Mbinguni.

Petro na Papa

Papa maana yake ni “Baba.” Baadhi ya watu humwita Papa kuwa “baba mtakatifu” watu hawa husema kwamba Petro alikuwa Papa wa kwanza wa Kanisa la kwanza, Petro alipokufa, aliwaachia wanadamu wengine uwezo au cheo chake. Maneno hayo si kweli. La! Maana Yesu mwenyewe aliwaambia wanafunzi wake: “Wala msimwite mtu Baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa Mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo,” Mt. 23:9-10.

Walakini, tangu siku za mitume baadhi ya watu wamemwasi Yesu wakitaka kuwaheshimu wanadamu na kuwapa cheo kinyume cha mapenzi ya Yesu. Paulo aliwalaumu watu hawa akisema:

“…Ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana kila mtu wa kwenu husema, mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo, na mimi ni wa Kefa (Petro), na mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Au Je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?……….basi ndugu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na apolo kwa ajili yenu, ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe.” 1 Kor. 1:11-13; 4:6.

Mkuu wa Kanisa

Yesu hakumfanya Petro wala mwanadamu ye yote kuwa mkuu wa Kanisa. La! Maana, ingawa Yesu yuko mbinguni, Yeye ni kiongozi pekee wa kanisa, katika Waefeso 1:21-23 twasoma kwamba Mungu akamweka Yesu: “Juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake.”

Tena twasoma: “Naye (Yesu) ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa; naye ni mwanzo ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.” Kol. 1:18.

Tazama! Mistari hii haisemi kwamba Yesu alikuwa kichwa cha Kanisa kana kwamba sasa amemwachia mtu mwingine cheo hiki. La! Bali inasema “naye ndiye kichwa.” Basi, ole wao wanaotaka kumnyang`anyayesu cheo chake! Maana Biblia yasema:

“Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia,” 2 Yn. 1:9.

Kufunga na Kufungua

Labda mtu atataka kubisha maneno yaliyoandikwa hapo juu akikumbuka jinsi Yesu alivyomwambia Petro “lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalo- lifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Mt. 16:18. Lakini kama tulivyosema huko juu maneno hayo hayakumfanya Petro kuwa mkuu kuliko mitume wengine. La! Yesu aliwapa mitume wote ahadi ile ile Mt. 18:18, “Amin, nawaambieni yo yote mtakayoyafunga duniani, yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”

Wala Yesu hakuwa na maana kwamba mitume walikuwa huru kufuata hiari yao katika kufunga na kufungua. La! Hasha. Yesu aliwaambia wazi wazi:

“Nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt. 10:18-20.

“Lakini huyo msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia …hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyahimili hivi sasa. Lakini Yeye atakapokuja, huyo Roho wa Kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.” Yn. 14:26; 16:12-14.

Tazama! Yesu alisema kwamba mwenye kufunga na kufungua alikuwa Roho Mtakatifu. Basi, Roho alitumia midomo ya mitume kutufungulia katika Sheria za Torati na kutufunga chini ya Sheria ya (Injili) ya Yesu (Rum. 7:6) Gal. 3:16, 19, 24, 35). Tena Yesu alisema kwamba Roho atawaongoza mitume wote katika kweli yote. Roho alimaliza kazi yake kabla mitume hawajafa. Wala mitume hawakubaki na uwezo wa kufunga au kufungua hata neno moja tangu alipomaliza kazi yake. La! Bali Paulo mwenyewe ametuonya:

“…Wapo watu wawatabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi (mitume) au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” Gal. 1:7-8.

Atukuzwe Yesu

Bila shaka mistari yote ya biblia ambayo tumeisoma katika kijitabu hiki imeonyesha wazi wazi kwamba Yesu ni kiongozi pekee wa Kanisa mpaka leo. Maneno yake yaliandikwa katika biblia kwa nguvu za roho ili watu wa kila taifa na kila karne waweze kumtii. Yesu alisema:

“Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Mt. 24:35.

“Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho,” Yn. 12:48.

Basi, hakuna mwanadamu aliyepewa mamlaka kubadili neno lo lote la Biblia. Hata hivyo, Yesu ametuonya kwamba watu watajaribu kutudanganya. Basi alisema:

“Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu …. waacheni hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.” Mt. 15:8-9, 14.