Na James M. Tolle (Mtafsiri Chris Mwakabanje)
Utangulizi:
1. Watu wengi wanapotembelea ibada za kanisa la Kristo kwa mara ya kwanza hustaajabia kitendo cha kutokuona ala za muziki ibadani.

2. Tunapaswa kuwa na majibu sahihi (1 Pet.3:15) kuhusu hili kama ilivyo katika mada mbalimbali zinazohusu Biblia.
a. Wasije wakadhani hatupendi tu kutumia vyombo vya muziki, au
b. Pengine, hatuna uwezo wa kununua ala za muziki.

3. Ala za muziki si miongoni mwa masuala yenye manufaa (expediency), bali ni mambo yanayogusa kanuni na taratibu (linga. 1 Kor.6:12).

4. Kanisa halifanyi mambo ambayo hulifurahisha, ama kufuata hekima za kibinadamu, bali kwa huzingatia mamlaka yatokayo juu (linga. Lk.20:1-8).

5. Je, Kristo ameamuru tutumie ala za muziki ibadani leo?
a. Tunapaswa kutambua ni wakati gani sheria inatufunga?
b. Je, maoni yana fungu gani katika ibada zetu?
c. Ni mambo gani yanachangia uimbaji bila kuvunja amri? (linga. 1Kor.6:12).

6. Kanisa la Kristo limefanya utafiti wa kina katika Neno la Mungu na kugundua kwamba hakuna amri, wala mfano wa Wakristo wakimwabudu Mungu huku wakitumia ala za muziki.
a. Kwa hiyo ni upotofu ambao haujatokana na mpango wa Mungu.
b. Kwa kuwa wanafunzi wengi wa Biblia wanashindwa kuthibitisha ndani ya Agano Jipya madai ya kutumia ala za muziki ibadani, basi aidha watakimbilia Agano la Kale au kwamba hakuna mahali Mungu amesema hapendi ala za muziki, n.k.

I. SHERIA YA IMANI

A. Tunaenenda kwa imani na wala si kwa kuona (2 Kor. 5:7).
1. Tunapata imani kwa njia ya kusikia neno la Kristo (Rum.10:17; Mt.17:5).

2. Kama tutafanya jambo bila kusikia kutoka ndani ya neno la Mungu, basi kibiblia hatuenendi kwa imani.

3. Pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu (Ebr.11:6).

B. Neno imba limetajwa mara 9, ukiondoa katika ufunuo lilivyotumika kwa namna ya mfano (Mt.26:30; Mdo.16:25; Rum.15:9; 1 Kor.14:14; Efe.5:19; Kol.3:16; Ebr.2:12; 13:15; Yako.5:13).

C. Hakuna shughuli yoyote inayolenga ibada itakayokubalika mbele za Mungu kama haijaagizwa naye.

1. Ibada inayokubalika mbele za Mungu inapaswa kuwa katika roho na kweli na wala si katika mwili, roho na kweli (Yoh. 4:24).
a. Ukweli ni neno la Mungu (Yoh.17:17).
b. Roho katika fungu hili ni utu wa ndani wa binadamu.

2. Tunapaswa kutofautisha huduma (service) na ibada (worship) – Rum.12:1-3.

3. Si kila kitu mwanadamu afanyacho ni ibada, kama Waislam wafundishavyo.

4. Ziko ibada aina nne:
a. Ibada katika roho na kweli (Yoh. 4:24)
b. Ibada ya kutungwa na wanadamu (Mt.15:8,9).
c. Ibada ya kujitungia (will-worship) – Kol.2:23. Matakwa ya mtu binafsi “arbitrary or self-devised worship.”
d. Ibada ya ujinga, huelewi mambo unayofanya ibadani (Mdo.17:22-28; Yoh.4:20-24).

D. Biblia inaagiza tunene mamoja wala pasiwepo na faraka kwa Wakristo (1Kor. 1:10).

1. Ikiwa Mungu anatuagiza kunia mamoja sisi kwa sisi na kuhitimu katika shauri moja; tukizingatia hayo ni vigumu tukatofautiana katika masuala ya msingi kabisa ya ibada (Filp.2:3-5; Rum.15:5).

2. Je, tunaweza kuwa na tumaini moja, imani moja, Bwana mmoja, Roho mmoja, ubatizo mmoja na Mungu mmoja, lakini si katika ibada moja? Efe.4:4-6.

3. Yesu aliliombea kanisa liwe na umoja, kama vile yeye alivyo na umoja na Baba (Yoh.17:20,21).

4. Watu hawajagawanyika katika masuala ambayo Yesu ameagiza, bali katika mambo ambayo hajaagiza. Hayo haswa ndiyo yanayotugawa kidini.
a. Hakuna anayepinga kuwa tunapaswa kuimba ibadani (Efe.5:19; Kol.3:16).
b. Mitume walifundisha mambo yote aliyoagiza Yesu (Mt.28:20; Yoh.16:13).
c. Roho Mtakatifu aliwaongoza mitume katika kweli yote. Ala za muziki si katika kweli yote aliyoifunua Roho Mtakatifu kwa mitume.
d. Mambo yote yafanyike kwa mamlaka ya Yesu Kristo (Kol.3:17).
i. Kuimba ni sharti kufanyike katika jina la Yesu, lakini kuimba pamoja na ala za muziki ni kinyume na mamlaka ya Yesu Kristo.
ii. Kwa kumjua (kujifunza) Kristo tumepewa mambo yote yapasayo uzima na utaua. Hatujifunzi popote Yesu na mitume wake wakitumia ala za muziki ibadani.

II. SHERIA YA IBADA
A. Kanuni za kweli za msingi kuhusu ibada ni muhimu sana kama ilivyo sheria ya imani; kwamba hakuna ibada yoyote itakayokubalika mbele za Mungu isiyoidhinishwa ndani ya Agano Jipya, Neno la Mungu.

B. Kanuni au sheria ya ibada imebainishwa katika Yoh. 4:24, “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

C. Ukweli ni nini? “Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli” (Yoh. 17:17).

1. Kwa kuwa wanadamu wanapaswa kuabudu katika kweli, na neno la Mungu ndio kweli, hivyo basi, wanapaswa kuabudu kulingana na neno linavyosema.

2. Ni mahali gani ndani ya Agano Jipya panatuamuru tutumie vyombo vya muziki? Hakuna hata mahali pamoja!

3. Kuimba, ukijumuisha na ala za muziki ni kuvunja sheria ya ibada kinyume na tulivyoagizwa katika Yoh. 4:24.

III. HISTORIA

A. Ala za muziki ziliingizwa baadaye sana katika ibada kanisani (647 B.K.). Hata hivyo hazikutumika hadi kufikia karne ya nane.

1. Paul Henry Lang, “Music in Westen Civilization,” uk. 53, 54: “Vyanzo vyote vya habari vinataja uimbaji kanisani, lakini tahadhari ichukuliwe panapotajwa sanaa nyingine ya muziki… Maendeleo ya muziki Magharibi ni ushawishi uliotokana na uimbaji bila ala za muziki katika Kanisa la Kikristo.”

2. Kurt Pahlem, “Music of the World,” uk. 27: “Kuimba kwa kupokezana mistari – na neno “chant” (sio ala) limetumika, kwa karne nyingi zilizopita kabla ya ala za muziki kuingizwa katika tuni (melody).”

3. Hugo Leichtentritt, “Music, History and Ideas,” uk. 34: “Hata hivyo, kuimba tu, na si kupiga ala za muziki, kulikubalika katika kanisa la awali.”

4. Emil Nauman, “The History of Music, Juzuu 1, uk. 177: “Pasipo shaka kabisa uimbaji wa awali katika ibada takatifu kila mahali ulikuwa bila ala za muziki.”

5. Dr. Frederic Louis Ritter, “History of Music from the Christian Era to the Present, uk. 28: “Hatuna taarifa yoyote kabisa hasa ya namna ya uimbaji kanisani ulivyokuwa katika ibada za kidini katika makusanyiko ya Kikristo. Walakini, hata hivyo, tunaona kuwa ulikuwa uimbaji bila ala za muziki.”

6. Frank Landon Humphreys, “Evolution of Church Music, uk. 42: “Moja ya taswira inayotofautisha dini ya Kikristo na zingine nyingi ni utulivu wake; ilikusudia kudhibiti ishara zinazojitokeza nje kupitia hisia za ndani. Tabia zisizo za kiustaarabu, tena za dini ya Kiyunani, wakicheza na kuamasika kwa mitindo mbalimbali ili kudhihirisha hisia zao… Wakristo karne ya kwanza walijizuia kuonesha ishara za kusisimka, tangu mwanzo kabisa, muziki waliotumia, uliendana na msingi wa dini yao – utulivu wa utu wa ndani. Uimbaji uliotumika katika ibada zao awali kabisa ulikuwa ni kuimba bila ala za muziki.”

7. George Park Fisher, “History of the Christian Church, uk. 65, 121: “Awali kabisa uimbaji kanisani sehemu kubwa ulihusisha kuimba Zaburi, ukistawi haswa sehemu za Shamu (Syria) na Alexandria. Uimbaji ulikuwa wa kawaida kabisa. Palikuwa na aina nyingine za uimbaji katika ibada ya Wakristo, kama inavyoelezwa na Pliny. Katika Antiokia walianzisha uimbaji wakitumia ala (antiphony), mhusika ni Ignatius… Muziki wa kanisa la kwanza kabisa ulikuwa wa kwaya ukijumuisha kusanyiko zima.”

8. John Kurts, “Church History, Juzuu 1, uk. 376: “Awali kabisa uimbaji kanisani ulikuwa wa kawaida, usio wa kisanaa, wa kughani. Lakini kuibuka kwa uasi kulipelekea kanisa la Orthodox litilie manani sanaa zaidi. Chrysostom alipaza sauti dhidi ya kuigia kwa muziki wa kidunia kanisani. Upinzani uliendelea ukipinga ala za muziki kujumuisha katika uimbaji.”

9. Joseph Bingham, “Works,” London Edition, Vol, II, uk. 482-884: “Muziki kanisani ni wa zamani kama vile walivyo mitume, lakini ala za muziki si hivyo… Matumizi ya ala za muziki, hakika, ni suala la hivi karibuni, na si katika ibada za kanisa… Eneo la Magharibu, ala hazikutambulikana hadi karne ya nane; maana kinanda cha kwanza kuonekana Ufaransa kilipelekwa na Kostatino Kopronymus, mfalme wa Uyunani kama zawadi kwa Mfalme Pepin… Lakini, kilitumika ukumbini kwa binti wa mfalme tu, hakikuingizwa kanisani; wala ala za muziki hazikupokelewa kabisa katika makanisa ya Uyunani, hazitajwi mahali popote katika Liturugia, aidha la kale au hata la sasa.

10. Edward Dickinson, “Music in the History of the Western Church,” uk. 55: “Mtakatifu Ambrose anaonesha kuwadharau watu wanaopiga kinubi na zeze badala ya kuimba tenzi za rohoni na zaburi; na Mtakatifu Augustine anawataka waumini wasikengeuke mioyoni mwao kwa kufuata ala za muziki. Miongozo ya kidini kwa Wakristo wa awali haikukubaliana na hilo (incongruity), na hata kuona ni kufuru, kutumia vitu ambavyo huamsha ashiki, matokeo ya ala za muziki kwa mambo yasiyoonekana, ibada ya kiroho. Shauku yao kuu kidini na kimaadili si kuongeza vichocheo vya nje; uimbaji bila ala ulikuwa ndio njia pekee ya kuelezea imani yao.”

B. Psallo na Psalmos

1. Kuna watu wanaojaribu kutetea matumizi ya ala za muziki ibadani kwa kutaja neno “psallo,” kwamba maana ya neno hili linauhusiano na ala za muziki.

2. Neno “psallo” limetokea mara tano katika Agano Jipya (Rum.15:9; 1 Kor.14:15 (mara mbili hapo); Efe.5:19; Yak.5:13, bila kuwa na maana tofauti kabisa, tafsiri (versions) zote zinazokubalika – King James, English Revised, American Standard, na Douay (Roman Catholic) – hulitafsiri neno “psallo” kuwa “imba, imba zaburi, imba sifa, lahani au tuni (melody).”

a. Hakuna hata tafsiri moja inayotafsiri kuwa ni kupiga ala za muziki.

b. Hata tafsiri maarufu za kisasa za siku hizi (Goodspeed, Weymouth, Moffat, na Knox) zote zinatafsiri “psallo” kimsingi sawa na hizo tafsiri zinazokubalika.

c. Watu waliotoa tafsiri hizo zote ni miongoni mwa watu waliobobea kitaaluma katika lugha ya Kiyunani, wangetafsiri kuwa ni ala kama ingemaanisha hivyo.

3. Moulton na Milligan, walioandika moja ya kamusi zinazotegemewa na kuaminiwa, wakishughulikia Kiyunani cha Agano Jipya, hulitafsiri neno “psallo” kama lilivyotumika katika Agano Jipya: kuimba tenzi za rohoni.”

4. Abbott-Smith anachangia akithibitisha maana iyo hiyo: “…katika A.J. kuimba tenzi za rohoni, kuimba sifa.” Uthabiti wa maelezo ni wa kweli tunapoangalia mazingira yaliyotumika ya “psallo” na waandishi wa A. J; maana mjadala si juu ya matumizi ya neno, bali lilimaanisha nini kwa waandishi walioandika Agano Jipya.

5. Matumizi ya neno katika Yakobo 5:13 ni mfano dhahiri kuonesha kwamba waandishi wa Agano Jipya hawakuwaza kabisa akilini mwao suala la ala za muziki kwa neno hilo: “ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi [psallo].” Kuimba, muziki bila ala za muziki, ni namna ya kudhihirisha furaha na shamrashamra, jambo ambalo wanadamu wanao uwezo wa kufanya hivyo katika maisha ya kila siku.

a. Kama neno “psallo” lilivyotumika katika Yakobo lingemaanisha ala za muziki, basi ili mtu mwenye moyo wa kuchangamka atii ingemlazimu kutafuta ala za muziki bila kujali yuko wapi – kazini, michezoni, nyumbani au akiwa safarini.

b. Maneno (Efe.5:19) “kumshangilia Bwana mioyoni mwenu” – Kiyunani “psallontes” kutoka neno “psallo.”

c. Katika Kol.3:16, “huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu ni sawa na “kumshangilia Bwana mioyoni mwenu.”

d. Nomino inaoungana na “psallo” ni “psalmos” iliyotafsiriwa kuwa zaburi katika Agano Jipya.

e. Dr. Marvin R. Vincent, akiandika katika “World Studies of the New Testament, uk. 506, anatoa maoni yafuatayo kuhusu matumizi ya neno zaburi katika Agano Jipya: “Zaburi asilia ziliimbwa zikiambatana na ala za muziki za nyuzi. Dhana ya kujumuisha ala za muziki ikapitwan na wakati, kisha kutajwa kwa neno zaburi katika Agano Jipya ni zaburi za Agano la Kale au utenzi wenye sifa hizo.”

f. Bagster anasema hivi kuhusu “psalmos,” “nyimbo takatifu, zaburi, 1 Kor.14:26; Efe.5:19;” n.k.

g. Mfano mwingine wa matumizi ya neno “psalmos” ni katika Luka 20:42, “Maana, Daudi mwenyewe asema katika chuo cha Zaburi…” Kama waandishi wangemaanisha “psalmos” kuwa ala za muziki, basi ingetafsiriwa hivi: “Maana, Daudi mwenyewe katika chuo cha kupiga ala za muziki, au chuo cha zaburi kutafsiriwa kwa kujumuishwa na ala za muziki. Kufikiri hivyo ni upuuzi!”

i) Kanisa la awali lilikuwa likifahamu vema Kiyunani na lilitumia lugha ya Kiyunani (hata Agano Jipya liliandikwa katika lugha hiyo), hawakuona vema neno “plasmos” na “psallo” kutafsiriwa kuwa ala za muziki.

ii) Wasomi walioandika kamusi za Kiyunani hawajatafsiri maneno “psalmos” na “psallo” kuwa ni kupinga ala za muziki.

iii) Waliotoa tafsiri (versions) maarufu pamoja na hizo zinazopendwa sana za kisasa, hawajatafsiri maneno “psalmos” na “psallo” kuwa ni ala za muziki.

iv) Kama maneno hayo yangemaanisha kupiga ala za muziki, basi kila Mkristo angepaswa kupiga ala za muziki kulingana na Efe.5;19 “Mkisemezana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni, huku mkiimba na kumshangilia Bwana mioyoni mwenu.” Na katika Kol.3;16, “Mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na tenzi na nyimbo za rohoni…”

IV. SABABU WATOAZO KUTUMIA ALA ZA MUZIKI

A. Hudai Agano jipya halisema ni makosa kutumia ala za muziki.
1. Katika chakula cha Bwana tumeamuriwa mkate usiotiwa chachu na mzao wa mzabibu. Je, ni sahihi kutumia nyama na viazi kwa sababu Bwana hajasema msitumie nyama na viazi mahali popote katika Agano Jipya?

2. Mungu alipowaambia Walawi wachukue moto madhahabuni kwa ajili ya kufukizia uvumba hekaluni, kwa kutaja hivyo alizuia moto mwingine wowote kutoka mahali popote pale (Law.10:1-2; 16:11,12).

3. Mungu ameagiza katika Agano Jipya tuimbe, mambo aliyonyamaza si ruhusa kwetu kabisa kuyafanya.

4. Kufundisha mambo ya Agano ya Kale ni kinyume na jinsi mitume walivyoamuriwa kufundisha, “Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi [mitume] hatukuwaagiza” (Mdo.15:24). Lazima tuheshimu Maandiko yanaponyamaza.

B. Watu hudai kwamba kwa kuwa Agano la Kale walitumia ala za muziki kwa nini leo tusitumie?
1. Yesu aliigongomelea torati msalabani na kuifuta isiwepo tena (Kol.2:14).
2. Leo, kanisa halimsikilizi Musa, bali Kristo (Yoh.1:17; Mt.17:5; 28:18).
3. Agano Jipya ni bora kuliko Agano la Kale (Ebr.8:6).
4. Ikiwa mtu anapenda kutumia vyombo vya muziki, basi inampasa kushika torati yote (Gal.3:10; Kumb.27:26; Law.18:5, n.k.).

C. Madai mengine ni suala la kuchangia tu uimbaji!
1. Wanaotoa madai haya hushindwa kutofautisha maneno kuchangia na kuongeza katika maagizo ya Mungu.

2. Neno mbao ni la jumla/ainasafu (generic). Kuna majina ya kipekee mengi kutoka ainasafu hiyo yanayobainisha mbao, kwa mfano mninga, mvule, msonobari, n.k.

3. Mwanzo 6:14, Nuhu aliambiwa atumie mvinje; kwa kuwa miti ni mingi duniani, unadhani angempendeza Mungu angetumia mti wa mninga, msonobari, mvule, n.k.?

4. Nuhu alifanya kila jambo aliloamuriwa na Mungu kikamilifu (linga. Mwa.6:22). Angetumia mti mwingine asingekuwa amechangia katika amri ya Mungu, bali angeongeza.

5. Mungu ametuagiza kuimba, unadhani atapendezwa tukiongeza kucheza, kupiga makofi, kupiga ngoma, gitaa, zeze, vinubi, n.k.?

6. Mungu hapendi wakati wote wanadamu waongeze wala kupunguza katika sheria zake (Kumb.4:2; 12:32; Mith.30:5,6; Ufu.22:18,19; 1 Kor.4:6).

7. Neno muziki ni neno la jumla/ainasafu. Kama Mungu angesema katika Agano Jipya pigeni muzika katika ibada, tungekuwa na uchaguzi: (1) muziki wa ala (2) sauti za vinywa vyetu, au (3) ala za muziki zikiambatana na sauti za binadamu.

8. Vitu vifaavyo, visivyo haribu amri ya kuimba ni: vitabu vya nyimbo, uma wa tuni (pitch pipe), kupanga sauti, pamoja na vyote visivyovunja amri ya kuimba.

9. Ala za muziki huwakilisha tendo lingine katika uimbaji tofauti kabisa na kutumia vitabu vya nyimbo, maiki, spika, n.k.

10. Mnyama ni neno la jumla/ainasafu (generic). Kuna wanyama wengi katika ainasafu hiyo kama vile: farasi, ng’ombe, kondoo, n.k.

a) Katika kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, Mungu aliwaagiza mnyama wa kutoa – mwana kondoo (Kut. 12:5).

b) Je, wasingevunja sheria kama wangetumia mnyama mwingine?

c) Au, ingekuwaje kama wangechinja mwanakondoo wakati wa Pasaka pamoja na wanyama wengine wasioagizwa?

11. “Neno niwaagizalo lo lote liangalieni kulifanya; usiliongeze, wala usilipunguze” (Kumb. 12:32).

D. Wengine hudai kuna ala za muziki mbinguni, kama alivyoona Yohana (Ufu.5:8; 14:1,2; 15:2).
1. Iwapo tutachukulia “wenye uhai wanne na wazee ishirini na nne … kila mmoja wao ana kinubi…” (5:8), kuwa ni lugha nyepesi ya kawaida, basi tunapaswa kutafsiri kuwa vitu halisi: wenye uhai wanne, wazee ishirini na wanne, sauti ya radi, vitasa vya dhahabu vilivyojaa manukato, mwanakondoo amesimama juu ya mlima Sayuni, kitu kama mfano wa bahari ya kioo iliyochangamana na moto!” (neno ‘kama’ huashiria tashibiha) – “kama sauti ya maji mengi, na kama sauti ya radi kuu, … kama sauti ya wapiga vinanda (14:2).

2. Suala hilo lingekuwa ni sahihi, basi tungengojea kufika mbinguni na kushuhudia ala hizo Mungu alizoziweka huko. Hapa mada yetu ni jinsi gani tumeagizwa kuimba kanisani! Kuna uhusiano gani mambo ya mbinguni na yale tuliyoagizwa hivi sasa kanisani?

E. Wengine hudai ala za muziki tunazofurahia majumbani kwa nini tusifurahie kanisani?
1. Kuna mambo mengi ambayo ni halali kufanyika majumbani, lakini hayawezi kufanywa ibadani; k.m. kuosha mikono, kula chakula, kuangalia Runinga, burudani mbalimbali, n.k.

2. Je, tuingize masuala ya majumbani mwetu katika ibada kwa Mungu? (linga. Kumb.12:13, 15).

F. Wengine hudai, makusanyiko yana watu wenye vipaji vya kupiga ala za Muziki, kwa nini tusiwatumie?
1. Vipi kuhusu wapishi wazuri wa keki watuandalie keki kwa ajili ya chakula cha Bwana?

2. Unaonaje kuhusu vijana wenye vipaji vya kuchekesha tuwatumie ibadani, watuburudishe badala ya kusikiliza mafundisho ya Biblia?