Yesu alipomchagua Simoni alimpa jina jingine la lugha ya Kiaramu akamwita Kefa. Maana yake katika Kiswahili ni jiwe (Yn. 1:40-42). Walakini lugha ambayo ilikuwa ikutumika zaidi katika siku za mitume ilikuwa Kiyunani. Katika Kiyunani jina Kefa linafasiriwa kuwa Petro. Watu wa siku zetu wamezoea sana jina Petro na, kwa hiyo, wengi wetu tumesahau kwamba katika Biblia Kefa na Simoni Petro ni mtu mmoja tu.
Petro na Mke Wake
“Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia (Yesu) habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia.” Mk. 1:30-31.
Mistari hii inaonyesha kwamba Petro alikuwa ameoa mke. Watu fulani hudhani kwamba mke wa Petro alikuwa amekufa kabla Yesu hajamchagua. Wazo hili si kweli. Mke wa Petro alikuwa akifuatana naye katika kazi yake. Maana Paulo aliuliza, “Hatuna uwezo kuchukua pamoja nasi mke aliye ndugu, kama wao mitume wengine, na ndugu wa Bwana, na Kefa (Yaani Petro)?” 1 Kor. 9:5.
Petro na Funguo za Ufalme
Tangu mwanzo, Petro alikuwa hodari sana katika kunena. Hata Yesu alipokuwa akiongea na mitume, mara kwa mara alikuwa ni Petro ambaye alitangulia kumjibu. Huenda ujasiri huu wa Petro ndiyo maana Yesu alimwambia katika Mathayo 16:19 kwamba atapewa “funguo za ufalme .” Basi, siku ya Pentekoste, Petro alitumia funguo hizo akiwaambia watu: “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu…… Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa… Bwana akalizidisha Kanisa kila siku kwa wale waliokuwa wakiokolewa”. Mdo. 2:38, 41, 47.
Watu waliookolewa waliingizwa katika Kanisa ambalo ndilo ufalme (soma Kol. 1:13-14 na Yn. 3:5). Basi, baada ya Petro kuufungua ufalme (Yaani, Kanisa) siku ya Pentekoste, Petro hakumwachia mwanadamu mwingine funguo hizo. La! Bali funguo zilirudi kwa Yesu huko Mbinguni. Soma maneno ya Yesu kwa Kanisa la Filadelfia katika Ufunuo 3:7-8.
Petro na Msingi wa Kanisa
Katika Mt. 16:18 Yesu alisema: “Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”
Kwa sababu ya maneno hayo, baadhi ya watu husema kwamba Petro ni mkuu na msingi wa Kanisa. Walakini Yesu hakusema kwamba Kanisa litajengwa juu ya Petro tu. La! Maana katika Efe. 2:20-22 twasoma “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. Katika Yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. Katika Yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika roho.”
Paulo alisema: “Maana sisi (mitume) tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi (Paulo) kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mweingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani Yesu Kristo,” 1 Kor. 3:9-11.
Mistari hii ya Biblia inaonyesha wazi wazi kwamba Kanisa limejengwa juu ya msingi wa mitume wote, wala si Petro tu. Tena msingi ule wa mitume haukuwa ni Petro bali ulikuwa Yesu mwenyewe. Kumbuka, katika Mathayo 16:18 Yesu hakusema kwamba atalijenga Kanisa juu ya jiwe (Petro) bali juu ya mwamba. Mwamba huu ni ukweli ule alioutaja Petro katika Mt. 16:16 alipomwambia Yesu, “Wewe ndiwe Kristo, mwana wa Mungu aliye hai.” Kwa hakika Kanisa limejengwa juu ya mwamba (ukweli) huu, maana mtu hawezi kuingia katika Kanisa bila kuamini kwanza kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
Petro na Mitume Wengine
Katika Mt. 16:19 Yesu alimwambia Petro “….Lo lote utakalo lifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Baadhi ya watu hudhani kwamba maneno hayo yalimfanya Petro kuwa mkuu kuliko mitume wengine. Walakini, wazo hili si kweli. Maana katika Mt. 18:18 Yesu aliwaambia mitume wote: “Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”
Yesu hakutaka kumfanya mtume mmoja awe mkuu kuliko wengine. Ebu! Tuone, siku moja mitume Yakobo na Yohana waliomba cheo kwa Yesu. Twasoma: “Wakamwambia, utujalie sisi tuketi mmoja mkono wako wa kuume na mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako… Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohana. Yesu akawaita, akawaambia, mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa nguvu na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote.” Mk. 10:37, 41-44.
Tena, twasoma: “Saa ile wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, amin, nawaambia msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi ye yote ajinyen- yekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni,” Mt. 18:1-4.
Petro na Uchungaji wa Kanisa
Watu wengine husema kwamba Yesu alimfanya Petro kuwa mkuu wa Kanisa alipomwambia “chunga kondoo zangu,” (Yn. 21:16). Walakini kazi hii ya kuchunga haikutolewa kwa Petro tu. La! Bali ni kazi ya wazee wote wa Kanisa (Mdo. 20:17, 18, 28). Petro mwenyewe amethibitisha ukweli huu, maana aliandika barua kwa wakristo akisema:
“Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni Kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa kwa moyo….. Na Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.” 1 Pet. 5:1, 2, 4.
Katika mistari hii Petro alionyesha wazi wazi kwamba hapakuwa na tofauti kati yake na wazee wengine wa Kanisa. Tena, alionyesha kwamba Mchungaji Mkuu ni Yesu atakayedhihirishwa kutoka Mbinguni.
Petro na Papa
Papa maana yake ni “Baba.” Baadhi ya watu humwita Papa kuwa “baba mtakatifu” watu hawa husema kwamba Petro alikuwa Papa wa kwanza wa Kanisa la kwanza, Petro alipokufa, aliwaachia wanadamu wengine uwezo au cheo chake. Maneno hayo si kweli. La! Maana Yesu mwenyewe aliwaambia wanafunzi wake: “Wala msimwite mtu Baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa Mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo,” Mt. 23:9-10.
Walakini, tangu siku za mitume baadhi ya watu wamemwasi Yesu wakitaka kuwaheshimu wanadamu na kuwapa cheo kinyume cha mapenzi ya Yesu. Paulo aliwalaumu watu hawa akisema:
“…Ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana kila mtu wa kwenu husema, mimi ni wa Paulo, mimi ni wa Apolo, na mimi ni wa Kefa (Petro), na mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulubiwa kwa ajili yenu? Au Je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?……….basi ndugu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na apolo kwa ajili yenu, ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe.” 1 Kor. 1:11-13; 4:6.
Mkuu wa Kanisa
Yesu hakumfanya Petro wala mwanadamu ye yote kuwa mkuu wa Kanisa. La! Maana, ingawa Yesu yuko mbinguni, Yeye ni kiongozi pekee wa kanisa, katika Waefeso 1:21-23 twasoma kwamba Mungu akamweka Yesu: “Juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya Kanisa; ambalo ndilo mwili wake.”
Tena twasoma: “Naye (Yesu) ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha Kanisa; naye ni mwanzo ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote.” Kol. 1:18.
Tazama! Mistari hii haisemi kwamba Yesu alikuwa kichwa cha Kanisa kana kwamba sasa amemwachia mtu mwingine cheo hiki. La! Bali inasema “naye ndiye kichwa.” Basi, ole wao wanaotaka kumnyang`anyayesu cheo chake! Maana Biblia yasema:
“Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia,” 2 Yn. 1:9.
Kufunga na Kufungua
Labda mtu atataka kubisha maneno yaliyoandikwa hapo juu akikumbuka jinsi Yesu alivyomwambia Petro “lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalo- lifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” Mt. 16:18. Lakini kama tulivyosema huko juu maneno hayo hayakumfanya Petro kuwa mkuu kuliko mitume wengine. La! Yesu aliwapa mitume wote ahadi ile ile Mt. 18:18, “Amin, nawaambieni yo yote mtakayoyafunga duniani, yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.”
Wala Yesu hakuwa na maana kwamba mitume walikuwa huru kufuata hiari yao katika kufunga na kufungua. La! Hasha. Yesu aliwaambia wazi wazi:
“Nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt. 10:18-20.
“Lakini huyo msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia …hata bado nikali ninayo mengi ya kuwaambia, lakini hamwezi kuyahimili hivi sasa. Lakini Yeye atakapokuja, huyo Roho wa Kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi; kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari.” Yn. 14:26; 16:12-14.
Tazama! Yesu alisema kwamba mwenye kufunga na kufungua alikuwa Roho Mtakatifu. Basi, Roho alitumia midomo ya mitume kutufungulia katika Sheria za Torati na kutufunga chini ya Sheria ya (Injili) ya Yesu (Rum. 7:6) Gal. 3:16, 19, 24, 35). Tena Yesu alisema kwamba Roho atawaongoza mitume wote katika kweli yote. Roho alimaliza kazi yake kabla mitume hawajafa. Wala mitume hawakubaki na uwezo wa kufunga au kufungua hata neno moja tangu alipomaliza kazi yake. La! Bali Paulo mwenyewe ametuonya:
“…Wapo watu wawatabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo. Lakini ijapokuwa sisi (mitume) au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe,” Gal. 1:7-8.
Atukuzwe Yesu
Bila shaka mistari yote ya biblia ambayo tumeisoma katika kijitabu hiki imeonyesha wazi wazi kwamba Yesu ni kiongozi pekee wa Kanisa mpaka leo. Maneno yake yaliandikwa katika biblia kwa nguvu za roho ili watu wa kila taifa na kila karne waweze kumtii. Yesu alisema:
“Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe,” Mt. 24:35.
“Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho,” Yn. 12:48.
Basi, hakuna mwanadamu aliyepewa mamlaka kubadili neno lo lote la Biblia. Hata hivyo, Yesu ametuonya kwamba watu watajaribu kutudanganya. Basi alisema:
“Watu hawa huniheshimu kwa midomo; ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu …. waacheni hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili.” Mt. 15:8-9, 14.